Tuesday, February 25, 2014

YANGA YATENGEWA MILION 100 KUWAUWA WAARABU

NA MARYLINE OLOTU
AL AHLY imepanga kuwasili nchini leo Jumanne tayari kuikabili Yanga Jumamosi hii kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Mwanaspoti linajua kwamba matajiri wa Jangwani wamepanda mzuka na kuwatengea wachezaji wao Sh100 milioni endapo wakishinda mchezo huo.
Yanga itavaana na mabingwa watetezi hao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kisha timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye huko Cairo, Misri.
Yanga ikiwa na kikosi chake kamili kitakachoongozwa na straika matata, Emmanuel Okwi, iko kambini Bagamoyo, Pwani, ikinoa makali.
Ingawa matajiri hao walidai kwamba ahadi yao ni siri mpaka wikiendi, habari za uhakika kutoka kwenye chanzo cha kuaminika ndani ya benchi la ufundi, zimeeleza kuwa fedha hizo zimeahidiwa ili kuongeza morali na kurahisisha mechi ya marudiano ugenini.
Tayari uongozi umewapa wachezaji hao zawadi ya Sh5 milioni baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 7-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara hivi karibuni.
Yanga ilipanga kuwapa Al Ahly Uwanja wa Karume kwa ajili ya mazoezi, lakini timu hiyo ikagoma na yenyewe ikaomba viwanja vya Gymkhana na Azam Complex ambako kote wamegonga mwamba hadi walipobahatika kwenye Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST).
Mechi ya Dar es Salaam itachezeshwa na Bazezew Belete wa Ethiopia na ya marudiano itachezeshwa na Mohamed Ragab wa Libya ambaye atasaidiwa na Fouad Fathi Farag kutoka Morocco.

0 comments:

Post a Comment