Friday, February 14, 2014

Lowassa, Sumaye, Ngeleja wajieleza Kamati ya Mangula



     Na Mariam George

          
 Mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye (kulia) na Edward Lowassa wakizungumza Mjini Dodoma jana kabla ya kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM. Picha na Adam Mzee  

.Waliowahi kuwa Mawaziri Wakuu; Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana walifika mbele ya Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM kutoa maelezo juu ya tuhuma za kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.
Mbali na wastaafu hao, mwingine ambaye jana alifika mbele ya kamati hiyo ambayo ilikuwa chini ya
 Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman
 Kinana ni Waziri wa Nishati wa zamani na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo aliyehudhuria kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa White House jana ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi. Wajumbe wengine ni Dk Maua Daftari, Shamsi Vuai Nahodha na Pindi Chana ambao hata hivyo, hawakuhudhuria
.
Hata hivyo, wanachama wengine watatu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Naibu wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambao wote wanatazamiwa kuitwa leo mbele ya kamati hiyo.
Vyanzo kutoka ndani ya chama hicho vilieleza kuwa Membe alikuwa katika ziara ya Rais Jakaya Kikwete na alitarajiwa kurejea nchini jana jioni.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa mahojiano ya makada hao watatu jana, Kinana alisema shughuli ya kuwahoji wengine itaendelea leo.
“Kazi haijakwisha, kesho (leo) tunaendelea.”Waliyosema baada ya kuhojiwa
Akiwa amevalia mavazi rasmi ya CCM, Lowassa alihojiwa kwa takriban saa moja na nusu kwani aliingia katika kikao hicho saa 4:56 asubuhi na kutoka saa 6:40 mchana akiwa ametumia takriban saa moja na nusu na alitoka akiwa mwenye furaha.
Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo Lowassa: “Mazungumzo yalikwenda vizuri. Yalikuwa na lengo la kujenga chama kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Lowassa huku akitabasamu.
Muda mfupi baada ya Lowassa kutoka, Sumaye aliingia kuanzia saa 6:46 na kutoka saa 8:05.
Baada ya kutoka, Sumaye pia hakuwa tayari kuzungumzia kuhusu mahojiano hayo... “Tunawasubiri wakubwa watakavyotoa jawabu.” Alipoulizwa sababu za kutumia muda mwingi katika kikao hicho alisema: “Tulikuwa tunakunywa chai.”

Chanzo:Mwananchi
 

0 comments:

Post a Comment