Saturday, February 15, 2014

MEZA YA UFUNDI: Soka la kuvutia limechezwa katika CHAN




Joseph Kanakamfumu
WATU wengi wanaopenda soka ni lazima watakuwa wanafuatilia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza katika ligi za nyumbani
(CHAN), michuano hiyo inafanyika nchini Afrika Kusini.

Kwa sasa imefikia hatua ya fainali, ni michuano mizuri na nadhani mwaka huu nimeona viwango vizuri vya timu za shiriki, hapa tunawazungumzia wanaopenda soka na si mashabiki wa mpira wa miguu. Hawa kwa ufupi wala hawajui kinachoendelea Bondeni kwa marehemu Madiba.

Hawa ni mashabiki wanaojua takwimu za mpira wa miguu lakini ufahamu wao upo katika Ligi Kuu England tu. Nilishawahi kuzungumzia ukoloni mamboleo katika michezo na hasa soka kitu ambacho kwangu sitaki kiendelee. Huko Kusini ndugu zangu umepigwa mpira wa maana na kama Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lingejaribu kidogo tu kuunda kombaini bora ya CHAN na ile ya AFCON nadhani madogo wa CHAN wangewatoa nishai wazee wa AFCON.

Sina maana kwenye CHAN hakuna vijeba! Wapo ila wengi wameendelea kucheza nyumbani na pengine hawakuwahi kupata bahati ya kutoka nje ya nchi zao. Kila mtu amewaona Zimbabwe! Wamebadilika sana walikuja Tanzania wakacheza na Taifa Stars mwaka jana, kila mtu aliona soka la kina Ngoma, Chipeta na wengineo. Soka lao lilikuwa la kuvutia sana na tusije kushangaa watakapoingia fainali za AFCON mwakani, tumewaona Uganda, wana kasi na pasi nzuri toka nyuma hadi mbele wamechangamka mno, wanajiamini na kila mtu ameonyesha uwezo wa kuucheza mpira, Nigeria wametoa somo na soka lao lilikuwa linavutia sana, wameonyesha nia ya dhati hasa walipocheza na Morocco huku wakiwa nyuma kwa goli tatu hadi kipindi cha kwanza kinakwisha lakini walikuja juu kipindi cha pili na kushinda kwa goli nne.

Nilivutiwa na Mali pia ingawa hawakufika mbali, tumewaona Mauritania, nchi ndogo lakini wamecheza CHAN kwa mafanikio ya kati. Wameonyesha mchezo mzuri sana lakini nadhani uzoefu umewatoa mashindanoni.
Tanzania tulishiriki hatua za awali na kutolewa mapema na Uganda huku tukiwa tumewahi kushiriki mara ya kwanza katika fainali za mwaka 2009 nchini Ivory Coast, licha ya kipindi kile hatua za kuingia CHAN zilikuwa ndefu kidogo maana tulicheza na nchi tatu za ukanda wetu kabla ya kufuzu. Mwaka jana kulikuwa na njia rahisi, tulicheza mkondo mmoja tu na Uganda tukatolewa.

Lakini ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati mwaka huu uliwakilishwa na Burundi, Ethiopia na Uganda zilizopangwa makundi tofauti. Hapa ndipo ninapoanza kujiuliza, kwa nini tunashindwa kufanya vizuri kwenye mashindano hata haya ambayo ni saizi yetu!

Angalau Uganda walipigana hadi siku ya mwisho ya mechi yao ya makundi, walicheza soka zuri na hiyo ilitokana na maandalizi yao ya awali, waliyatumia mashindano ya Challenge kule Kenya kuiandaa timu yao. Wakati wakifanya hivyo nchi ambayo kila mfuatiliaji wa mashindano ya Afrika alijua ingefanya vizuri ni Ethiopia iliyowatoa jasho Nigeria wakati wakigombea tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Brazil, lakini walilewa sifa na badala kuitumia Challenge kuiandaa timu yao, wao waliwapumzisha wachezaji wao na kuwaleta yosso!
Ndio maana huwa nashauri hata timu za Tanzania zinazotumia msemo wa kukuza vijana, si kwamba ukuze tu kila mwaka, na pale unapotakiwa kupata faida ya kukuza unawaacha hao na unaanza kukuza wengine, hawa Ethiopia ndio nadhani wangebeba mioyo yetu ya mafanikio kwa timu za ukanda huu.







0 comments:

Post a Comment