Thursday, September 25, 2014

UTATA KESI YA KUBENEA KUPINGA BUNGE MAALUM




KESI ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Said Kubenea akihoji mamlaka ya Bunge la Katiba, jana imeibua utata baada ya majaji kubaini maana mbili tofauti ya kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.

Mmoja wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Aloysius Mujulizi alibaini hilo wakati Kubenea akiwasilisha hoja zake kupitia kwa mawakili wake, Peter Kibatala na Mabere Marando katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Majaji w
engine wanaounda jopo hilo, linalosikiliza kesi hiyo ni Augustino Mwarija na Dk Fauz Twaib. Jaji Mujulizi alisema kuna utofauti wa maana ya kifungu hicho katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili, jambo lililosababisha Kibatala asome kifungu hicho kilivyoandikwa kwa lugha hizo. Katika Kiswahili kifungu hicho kimeandikwa:

“Mamlaka ya Bunge Maalumu ya kupitisha masharti ya Katiba yanayopendekezwa, yatatekelezwa baada ya Rasimu ya Katiba kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume na kupitishwa na Bunge.”
Wakati kwa tafsiri ya Kiingereza, imeandikwa Bunge Maalumu la Katiba litatekeleza madaraka yake kwa kuongozwa na kujikita kwenye Rasimu itakayokuwa imewasilishwa na Mwenyekiti wa Tume na kupitishwa na Bunge.
Wakili Marando alidai jambo hilo, linatokana na Kiingereza kibovu na kutoandikwa kwa ufanisi, lakini licha ya upungufu huo bado bunge hilo linatakiwa kufanyakazi kwa mujibu wa misingi ya rasimu ya Katiba
.
Aidha, hakuna kifungu chochote kinachoruhusu bunge hilo kutofuata rasimu, pia halina mamlaka ya kukusanya maoni mapya, wakifanya hivyo watakuwa wanakwenda kinyume na maoni ya wananchi, lakini wajumbe hao wanakusanya maoni yao na hivi karibuni Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta aliwaita watu watoe maoni yao.

Kibatala aliiomba Mahakama itoe tafsiri ya kifungu hicho, kwasababu kutokana na mgongano wa tafsiri hiyo, taifa limegawanyika na hata wajumbe wa bunge hilo wametengana.

Alidai kundi moja la wajumbe la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), limegoma kuendelea na vikao hivyo, wakati kundi linaloendelea na vikao linakusanya maoni mapya, kwa madai kifungu hicho kinawapa mamlaka.
Akijibu hoja hizo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alidai kuwa vifungu hivyo, havitofautiani kwa kuwa vinaleta maana moja, lakini kuna tatizo la maandishi na matumizi ya lugha.

Aliongeza kuwa Bunge lilipewa rasimu kama nyaraka ya kufanyia kazi na hakuna ulazima wa kufuata kifungu hicho. Kubenea alifungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba Mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba, kwa kuzingatia Kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.

Aidha, anaiomba Mahakama itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba, iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.HABARI  NA  WINLADY  JOHANESS

0 comments:

Post a Comment