Thursday, September 25, 2014

CHADEMA KILOSA WABAINI MCHEZO MCHAFU


 
UONGOZI mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Kilosa mkoani Morogoro umeanza kazi kwa kunasa makada wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Magomeni wilayani hapa wakiwa na nyaraka za serikali kinyume cha sheria wakiandikisha majina ya watu.

Wakizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Kilosa, Seleman Simba na Katibu wa Jimbo la Kilosa Kati, Mussa Ngongi, kwa nyakati tofauti walisema makada hao wa CCM waliwanasa Septemba 7 mchana wakiendelea na zoezi hilo la uandikiashaji.

“Kisheria zoezi lilipaswa kufanywa na maofisa watendaji wakishirikiana na wenyeviti wa vitongoji, tofauti na hivyo uongozi wa halmashauri kwa makusudi umegawa kwa makada wa CCM vitabu vya kuandikisha majina ya wakazi vitongoji…kwa mtazamo wetu hii inafanyika makusudi kuiandalia CCM ushindi katika chaguzi zijazo,” alifafanua Ngongi.

Viongozi hao, walisema mbali na zoezi hilo kushitukiwa kwa kupewa makada wa CCM kuliendesha badala ya watumishi wa serikali, walilishitukia kutokana na lilivyokuwa likiendeshwa kwa ubaguzi likiwatenga wenye itikadi tofauti na CCM na wenye misimamo tofauti.

Walibainisha kuwa kilichowashangaza zaidi ni hata baada ya suala hilo kufikishwa kituo kikubwa cha polisi wilayani hapa, Polisi akiwemo mkuu wa kituo hicho walilazimisha suala hilo kumalizwa kwa mazungumzo badala ya sheria kufuta mkondo wake.

Katika ufafanuzi wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Idd Mshili, mbali na kukiri kuwepo kwa zoezi la utambuzi wa wakazi unaofanyika kila baada ya miezi mitatu, alikana halmashauri hiyo kutoa kazi hiyo kwa makada wa CCM zaidi ya maofisa watendaji anaowatambua kisheria.HABARI  NA  WINLADY  JOHANESS

0 comments:

Post a Comment