WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk.
Abdallah Kigoda, amewataka Watanzania kuacha kununua bidhaa zisizosindikwa
kwani hupunguza pato la taifa na kuchangia kupungua kwa ajira nchini.
Alisema hayo jana katika ufunguzi wa
maonesho ya bidhaa kutoka China, ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya wanunuzi wa
bara la Afrika.
Alisisitiza kuwa, urafiki wa
Tanzania na China unaimarika kutokana na juhudi mbali mbali zinazofanywa na
serikali zote mbili hasa katika biashara.
“Tumezungumza na Serikali ya China
kuona ni namna gani itaweza kutusaidia kutatua changamoto kubwa zinazotokana na
uchumi, kwani wenzetu (China) wako mbele kimaendeleo zaidi yetu,” alisema Dk.
Kigoda.
Akizungumzia changamoto ya kuingizwa
kwa bidhaa zisizo bora kutoka uchina Dk. Kigoda, alisema serikali inashindwa
kudhibiti wafanyabiashara wasio waaminifu ambao hushiriki vitendo hivyo
kutokana na wingi wa mipaka inayoizunguka nchi na kukosa watendaji wa kutosha
katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Aidha, Balozi wa China nchini Lu
Youqing, alisema Watanzania wanakaribishwa kutangaza bidhaa nchini China katika
kukuza soko la bidhaa zao.
“Kwa sasa bidhaa za Uchina zinauzwa
kwa bei nafuu ili kuendana na hali ya kimaisha ya Watanzania wengi katika kusaidia
upatikanaji wake bila kubagua hali ya mtu,” Alisema Balozi Youqing.
Maonyesho haya yaliyofunguliwa rasmi
jijini Dar es Salaam jana, yataendelea kufanyika hadi mwishoni mwa wiki hii nia
ikiwa ni kutoa fursa kwa Watanzania kufahamu bidhaa zinazozalishwa kutoka
China.
Habari na Everline bakari,
0 comments:
Post a Comment