Ndege za kivita za Israel zimeyashambulia maeneo 29 ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo (13.03.2014) kujibu mashambulizi ya maroketi ya Wapalestina katika taifa hilo la kiyahudi.
Wapalestina walioshuhudia, pamoja na mpigaji picha wa shirika la habari
la AFP wamesema ndege za kivita zilizishambulia kambi za watawala wa
chama cha Hamas na kitengo cha kijeshi cha kundi la Islamic Jihad,
Al-Quds Brigades, ambalo limedai kuhusika na mashambulizi hayo.
Taarifa ya jeshi la Israel imesema siku ya Jumatano usiku kwamba mabaki
ya maroketi 60 yamepatikana, matano kati ya hayo yakisemekana kuanguka
katika maeneo yenye watu wengi. Ripoti hiyo imemnukuu luteni kanali
Peter Lerner akisema operesheni hiyo imefanyika kwa umakini mkubwa na
bila kuchelewa. "Tumeilenga miundombinu inayowasaidia magaidi wakati
wanapopata mafunzo, kupanga na kutekeleza mashambulizi yao.
Hawataruhusiwa kupanga njama katika usalama wa mahekalu ya magaidi,"
ikaendelea kusema ripoti hiyo.
Wapiganaji wa Al-Quds Brigades wamesema wamefyetua maroketi 90 nchini
Israel kulipiza kisasi mauaji ya wenzao watatu waliouwawa siku ya
Jumanne kusini mwa Gaza katika shambulizi la angani la jeshi la Israel.
Wapiganaji hao wametoa tamko wakisema mashambulizi yao yataendelea
kujibu hujuma ya Israel ya Jumanne wiki hii. Hamas imeionya Israel dhidi
ya kuchochea makabiliano.
0 comments:
Post a Comment