Tuesday, October 29, 2013

KATIBA MOTO TENA BUNGENI:::Kura ya maoni, muswada uliosainiwa kutikisa BUNGE!!


Spika wa Bunge,Anne Makinda
Mkutano wa 13 wa Bunge unaanza leo mjini hapa, huku suala la Katiba ya mpya ya Tanzania ambayo mchakato wa mabadiliko yake unaendelea, likitarajia kuutawala na kuwagawa wabunge kwa mara nyingine. 
Hali hiyo inatarajiwa kujitokeza iwapo serikali itatekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya kamati yake na ile ya vyama vya siasa ya kuurudisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013 kwa hati ya dharura, ili kutoa fursa kwa wabunge kujadili mapendekezo ya kuuboresha. 
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa serikalini kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Wiliam Lukuvi, na vyama vya siasa vyenye uwakilishi na visivyokuwa na uwakilishi bungeni, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni. 
Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Deogratias Egidio, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa serikali imesema itaupeleka bungeni muswada huo ajili ya kujadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa sasa. 
Hata hivyo, alisema hadi jana Bunge lilikuwa bado halijaupokea muswada huo kutoka kwa serikali.“Serikali imesema italeta (muswada huo), lakini Bunge halijapokea,” alisema Egidio. 
Katika mkutano wa 12 wa Bunge, wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, walisusia na kutoka nje wakati wa kujadili na kupitishwa kwa muswada huo wakidai kuwa una kasoro kadhaa. 
Kasoro hizo walizitaja kuwa ni kutoshirikishwa kwa Zanzibar , madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha Rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni. 
Vyama hivyo licha ya wabunge wake kususia Bunge, pia viliunda ushirikiano wa kupinga mchakato wa Katiba kwa maelezo kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM). 
Wenyeviti wa vyama hivyo; Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi walifanya mikutano ya hadhara jijiji Dar es Salaam na Zanzibar kwa nyakati tofauti. 
Awali, vyama hivyo viliandaa maandamano ya nchi nzima na baadaye kufanya mikutano mingine katika mikoa yote kuwashawishi wananchi waukatae mchakato huo. 
Aidha, vyama hivyo na makundi ya wanaharakati walimtaka Rais Kikwete asiusaini muswada huo kwa maelezo kuwa utaleta Katiba mbovu, ambayo haina maslahi kwa taifa. 
Muswada huo, ambao ulipitishwa na Bunge Septemba 6, mwaka huu, katika Mkutano wake wa 12, ulikwisha kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuanza kutumika kuwa sheria rasmi. 
Vyama hivyo viliwasilisha mapendekezo ya kuuboresha muswada huo, huku vikiendelea na vikao kujadili namna ya kupata maridhiano ya kitaifa chini ya kaulimbiu “ Tanzania Kwanza ”, katika kuelekea kwenye Bunge Maalumu la Katiba, linalotarajiwa kuanza Desemba, mwaka huu. 
Hatua hiyo ilichukuliwa na vyama hivyo siku chache baada ya mazungumzo kati ya Rais Kikwete na vyama vyenye uwakilishi bungeni, yaliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, Oktoba 15, mwaka huu, na kufikia makubaliano makuu mawili.

La kwanza, vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, kuyawasilisha haraka serikalini ili kutafuta namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo. 
La pili, vyama hivyo, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato mabadiliko ya katiba ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali wa taifa 
Katika makubaliano hayo, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kilipewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini. 
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baadaye, mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi ulimalizika na pande mbili hizo kukubaliana mambo hayo. 
Oktoba 22, mwaka huu, kuwa kamati ya serikali na ya vyama hivyo walikutana na walikubaliana muswada huo urudishwe bungeni katika Mkutano wa sasa wa Bunge kwa hati ya dharura. 
Vikao hivyo vilizingatia makubaliano yaliyofikiwa kati yao na Rais Kikwete, Ikulu. 
Makubaliano hayo ni pamoja na vyama vyote kukaa meza moja na kufikia maridhiano ya kutanguliza mbele maslahi ya Taifa chini ya kaulimbiu ya “Tanzania Kwanza” kabla ya kitu kingine chochote, zikiwamo itikadi na tofauti za kisiasa. 
Mbali na hilo, katika mazungumzo na Rais Kikwete, pia walikubaliana kupanua wigo zaidi wa kuboresha mchakato wa mabadiliko ya Katiba, badala ya vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi pekee kama ilivyokuwa awali. 
Aidha, ilikubaliwa kuwa na mchakato shirikishi usiokuwa na ubabe.

MPANGO WA SERIKALI
Egidio pia alisema kutokana na mabadiliko ya Kalenda ya Mkutano Bajeti ya Serikali na pia kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za  Bunge toleo la 2013, Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango ili kutekeleza matakwa ya Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kujadili na kuishauri serikali juu ya mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015. 
Alisema Bunge linategemewa kuujadili mpango huu kwa siku tano.
  MISWADA YA SHERIA YA SERIKALI
Alisema pi miswada minne ya sheria ipo katika hatua za mwisho za kufanyiwa uchambuzi na Kamati za Bunge na pindi itakapokuwa tayari itasomwa kwa mara ya pili na majadiliano yataendelea kwa hatua zake zote. 
Aliitaja miswada hiyo kuwa ni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013, Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa Mwaka 2013.
  MASWALI KWA WAZIRI MKUU
Egidio alisema kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 38, Waziri Mkuu ataulizwa maswali ya msingi 16 katika Kipindi cha Maswali ya papo kwa papo.

Maswali ya kawaida
Pia alisema kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 39, jumla ya maswali 125 ya kawaida yataulizwa na kujibiwa. 
Egidio alisema pamoja na shughuli zilizoorodheshwa, Bunge linaweza kufanya shughuli yoyote, ambayo haipo kwenye orodha hiyo ya awali ikiwa itakidhi matakwa ya kikanuni kama litaona inafaa. 
Miongoni mwa mambo yaliyotarajiwa kuwamo kwenye orodha ya shughuli za Mkutano wa sasa wa Bunge na kujadiliwa na wabunge, ni muswada binafsi uliowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye anataka Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ifutwe. 
Kwa mujibu wa Zitto, madhumuni ya muswada huo ni kufuta sheria hiyo kwa sababu inakinzana na Katiba ya nchi kuhusu haki za raia kupata habari. Alisema sheria hiyo iliorodheshwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyokusanya maoni ya wananchi juu ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kuwa ni sheria kandamizi.
 
CHANZO: NIPASHE
POSTED BY:Emanuel Onesmo Ndanshau

0 comments:

Post a Comment