Tuesday, October 29, 2013

SAMSON MWIGAMBA AMWAGA VIELELEZO KUTHIBITISHA MADAI YAKE .... MBOWE, LEMA NA MNYIKA WAMESHIKWA PABAYA ... RIPOTI KAMILI HII HAPA!!


SAMSON MWIGAMBA
Kwa siku za karibuni, umezuka mjadala mkali ndani ya mtandao huu pendwa hasa baada ya Samson Mwigamba ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha kuwatuhumu viongozi wa kitaifa wa CHADEMA kuwa wamebadilisha katiba kinyemela kwa kuondoa ukomo wa uongozi wa awamu mbili ili waendelee kubaki madarakani. Mwigamba ametoa shutuma hizo akitumia jina bandia la Maskini Mkulima. Katika shutuma zake Mwigamba amesema yafuatayo;

Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano. Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa. Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa nayenye athari zisizomithirika kwa chama.

Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.

Mara baada ya taarifa hiyo ambayo ilibebwa kwa jina la Wito kwa wana CHADEMA wote! ambayo ilieleza madhaifu ya chama na kubadilishwa kwa vipengele vya katiba kinyemela, Dr Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA alitoa ufafanuzi ufuatao;

Nataka kuwahakikishia wanachadema wote, kuwa nilikuwepo nimekuwa ndani ya Chadema kuanzia 1998 ambapo nilikuwa Makamu Mwenyekiti Bara, na baadaye 2003 Kaimu Katibu Mkuu, na hatimaye Katibu Mkuu. Hivyo nimeshiriki kikamilifu kuandaa Katiba ya 2004 na pia Katiba ya 2006 baada ya Rebranding ya Chama. Nataka niwahakikishie wanachadema, hakuna toleo lolote la Katiba ndani ya Chadema imeweka " muda wa Uongozi kuwa vipindi viwili tu", kuanzia Katiba aliyoiasisi Mzee Mtei na kupitishwa na Mkutano Mkuu, wala si ya 2004 au ya 2006. Kama kuna mtu anasema ilikuwepo na imeondolewa kinyemela, basi aonyeshe kifungu hicho kwenye Katiba yeyote ile, au miniti za kikao chochote kile.

Hata hivyo, majibu hayo ya Dr Slaa yanaonekana kutofautiana na yale ya JOHN MNYIKA aliposema kuwa kwenye katiba ya 2004 kipengele cha ukomo wa uongozi kiliwekwa lakini hakikuingizwa kwenye katiba ya 2006. John Mnyika anasema;
Kuhusu Katiba, nina nakala mango (hard copy) tu ya katiba ya 2004, ilikuwa na kipengele cha vipindi viwili vya nafasi ile ile. Hata hivyo, katiba mpya iliyoandikwa mwaka 2006 haikuwa na kipengele hicho. Hivyo, sio kwamba kimeondolewa kinyemela ila hakikuwepo kwenye katiba mpya. JJ

Baada ya malumbano hayo, nilifanya utafiti mdogo ili kujiridhisha na hoja zilizotolewa na viongozi hao. kwa msaada mkubwa kutoka kwa wadau muhimu ndani ya CHADEMA, nimefanikiwa kupata nyaraka zifuatazo
  1. Nakala ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2004 iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza
  2. Nakala ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006 iliyoandikwa kwa lugha ya kiswahili
  3. Muhtasari wa Mkutano Mkuu Maalum wa CHADEMA uliofanyika katika ukumbi wa PTA Dar es Salaam tarehe 13, Agosti 2006

Nitajaribu kuweka vipengele muhimu mahsusi kwa mjadala huu. Nitajikita kwenye hoja moja tu ya Mwigamba kuwa Viongozi wamefanya marekebisho ya katiba kinyemela kwa kuondoa ukomo wa madaraka ili waendelee kuwepo madarakani.

Katiba ya mwaka 2004 ipo wazi kabisa katika hoja ya ukomo wa madaraka. Ibara ya 6.3.2 kipengele cha (c) kinasema ifuatavyo; ''Leaders who finish their term of office can be eligible for re-election provided he qualifies but no leader can hold the same post at the same level of the party structure for more than two terms. Kutokana na kipengele hiki, kauli ya Dr Slaa kuwa hakuna katiba ya CHADEMA iliyoweka ukomo wa madaraka ni ya kushangaza ikizingatiwa kuwa yeye ni Katibu Mkuu na hakupaswa kusema uongo mbele ya watu ambao wanaelewa mengi kuhusu katiba hizo.

Katika Mkutano Mkuu Maalum wa mwaka 2006 ambao ulikuwa na ajenda 4 ambazo ni;
  1. Kufungua Mkutano
  2. Maboresho ya Katiba
  3. Maazimio juu ya Katiba Mpya na
  4. Kufunga Kikao

ulijadili vifungu 10 ambavyo vimefanyiwa marekebisho kutoka kwenye katiba ya 2004. Kati ya vipengele hivyo, kipengele cha ukomo wa madaraka hakimo na hii ni kusema kuwa hoja hiyo haikuwa na marekebisho. Vipengele vilivyofanyiwa marekebisho kwa mujibu wa muhtasari huo vimeambatishwa na taarifa hii.

Katiba ya Mwaka 2006 ndiyo inayolalamikiwa kuchakachuliwa kwa vile kipengele cha ukomo wa madaraka hakimo na hakuna mkutano uliojadili hoja hiyo. Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa hoja za Samson Mwigamba ni sahihi na viongozi wa CHADEMA hususan DR WILBROAD SLAA NA JOHN MNYIKA wametoa majibu ya uongo kupinga hoja za kweli. kwa mantiki hiyo, ni wazi kuwa katiba imechakachuliwa kwa maslahi ya wanaotetea uchakachuaji huo.
CHANZO:JAMII FORUM
posted by:Emanuel Onesmo Ndanshau

0 comments:

Post a Comment