Friday, June 6, 2014

Warioba azishukia Ukawa, CCM kuepusha migogoro isiyo na tija



 

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewashauri wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CCM kuacha kuzunguka mikoani kufanya mikutano inayoeleza misimamo yao kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa haina tija kwa taifa.
Ameonya kuwa mikutano hiyo inajenga mwelekeo mbaya kwa taifa na kuhatarisha mchakato wa Katiba na kuzitaka pande hizo kumaliza tofauti zao.
Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Warioba alisema: “Kwa mustakabali mwema wa taifa, ni muhimu makundi haya ‘ya-resolve’ (yamalize), matatizo yaliyopo kabla ya Agosti, ili Bunge Maalumu la Katiba likirejea, wote washiriki na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya. Hili ni kwa masilahi ya taifa.”
Kauli ya Waziri Mkuu huyo mstaafu ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu, imekuja huku makundi ya Ukawa linaloundwa na wabunge wengi wa upinzani na viongozi wa CCM wakiendelea kung’ang’ania misimamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Wakati CCM ikipinga mapendekezo ya kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu uliomo kwenye Rasimu, Ukawa unaunga mkono mapendekezo hayo.
Aprili 16, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliiongoza Ukawa kutoka ndani ya Bunge la Katiba baada ya kumaliza kuchangia mjadala huo, kwa madai ya kutokutendewa haki na CCM katika mambo mbalimbali ikiwamo kupinga mapendekezo ya upinzani hata yale ya msingi akisema hawawezi kuwa sehemu ya watu wanaosambaza chuki na kuwa sehemu ya kuibomoa nchi.
Siku chache baadaye, Ukawa ulianza mikutano nchi nzima kwa kile ulichodai kuwaeleza wananchi namna CCM inavyotaka kuchakachua maoni yao yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kwa upande wake, CCM imekuwa ikifanya mikutano kueleza msimamo na sababu za kutaka kuendelea kwa muundo wa serikali mbili.
Jaji Warioba alisema makundi hayo yana nafasi ya kumaliza tofauti zao kabla ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza tena vikao vyake, hivyo kuliwezesha taifa kupata Katiba Mpya.
Alisema makundi hayo yasipopatana yanaweza kuhatarisha mustakabali wa taifa hata amani iliyopo.
Alionya kuwa amani iliyopo nchini ikivurugika kwa sababu yoyote ni vigumu kuirejesha na kwamba watakaotaabika ni wananchi.
Jaji Warioba ambaye aliwahi kuongoza Tume ya Rushwa iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alisema amani ya Tanzania ikivurugika kutokana na makundi kupingana katika mchakato wa Katiba wanasiasa ndio watakaonyooshewa vidole.
 credit: Mwananchi
Augustina kawau.

0 comments:

Post a Comment