Jeshi la Polisi nchini
limetangaza zawadi ya Sh. milioni 10 kwa atakayewezesha kukamatwa kwa
watu waliotumia mabomu kulipua baa ya Night Park mwishoni mwa wiki
iliyopita. Katika mlipuko huo, watu 17 wameripotiwa kujeruhiwa kati ya
hao, waliobaki wodini kuendelea na matibabu ni nane baada ya wengine
kuruhusiwa.Wanaondelea na matibabu ni Evance Maleko, Evarist Richard,
Petro James, Christian Zakaria, Pius Shayo, Antelus Ishengoma, Sudi
Ramadhani na Mariam Hansi aliyeko hospitali ya Selian.Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Isaya Mngulu, alisema
uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo umebaini kuwa bomu lililolipuliwa
Aprili 13, mwaka huu, saa 1:30 asubuhi kwenye baa hiyo, ni la
kutengenezwa kienyeji.Mngulu alisema wataalamu wa mabomu waligundua bomu
lingine lililokuwa kwenye mkoba ulioegeshwa kwenye kiti katika baa ya
Washington, pembeni mwa baa hiyo. “Bomu hili tumeligundua baada ya
tukio hili kutokea na saa sita usiku tukaligundua, lakini halijalipuka
na tunalo kwa ajili ya kuchunguza tujue limetengenezwa kwa kutumia vifaa
gani,” alisema.Alisema hata bomu hilo ni la kutengenezwa kienyeji,
jambo lililowafanya waelewe hata hilo lililolipuka ni la kienyeji.Mngulu
alisema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo nchini kwa sasa, ni vema
wananchi na hasa wale ambao wapo maeneo ya mkusanyiko, wakachukua
tahadhari za uhakika, kwani siyo vema kumwamini hata rafiki yako.“Ni
vizuri ukajiridhisha alichobeba rafiki yako kwenye mkoba na ukitilia
wasiwasi bora utoe taarifa polisi na siyo kukaa kimya hadi madhara
yakatokea,” alisema.Alitoa rai kwa wamiliki wa kumbi za starehe,
makanisani, misikitini na maeneo ya mikusanyiko kujitahidi kuweka kifaa
cha CCTV ili kuwezesha kubaini wahalifu pale uuhalifu unapotokea.Alisema
hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kwa kuwa wana
kifaa cha CCTV kilichofungwa Night Park, wana hakika muhusika
atapatikana. Alisema matukio ya milipuko ni mengi kutokea nchini kwa
sasa na yanatokea maeneo mbalimbali na siyo Arusha peke yake, isipokuwa
wote wanaokamatwa na milipuko hiyo kama Dar es Salaam na Tanga ni vijana
wadogo ambao hawajawahi hata kupita jeshini.Kuhusu Sikukuu za Pasaka,
alisema kila mkoa umepewa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi kutumia mbinu
zao zote na vifaa walivyonavyo kama farasi na mbwa ili kulinda usalama
wa ibada za sikukuu hizo.
0 comments:
Post a Comment